USOMAJI WA DIRA ZA MAJI

  1.  Wateja wote wanaotumia mita/dira za maji, mita zao zitasomwa mara moja ndani ya mwezi mmoja na kwa wateja wakubwa zaidi ya mara moja inapoonekana uhitaji wa kufanya hivyo, kwa ajili ya kutayarisha Ankara. Kama mita haitasomwa katika mwezi mmoja na kama wakati wa usomaji, mita hiyo itakutwa/itabainika kuwa mbovu matumizi ya mteja yatakadiriwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za maji.
  2. Mteja anahimizwa kutoa taarifa haraka kwenye ofisi za Mamlaka kwa tatizo lolote linalohusiana na mita yake.
  3. Usomaji wa mita wa ziada utafanyika kama mteja anahama kwenye sehemu iliyopo na mteja mwingine anaingia, au kusitisha huduma kwa muda kumaliza mkataba wa ukazi au uraia wa nchi, au kuuza eneo au kufunga kabisa kampuni ili baada ya kubadilisha mita, au kama mteja atataka mita yake isomwe kwa ajili ya marekebisho ya Ankara au malipo na itakapo lazimu kubadilisha dira nyingine.
  4. Wamiliki wa nyumba/majengo wanaotarajia kubadilisha umiliki au matumizi ya nyumba/majengo yao kama vile kutoka matumizi ya nyumbani kwenda matumizi mengine kama vile biashara, kiwanda, ujenzi, taasisi, n.k lazima watoe taarifa angalau siku 30 kabla ya mabadiliko hayo hayajafanyika katika ofisi za BUWSSA ili abadilishiwe gharama za matumizi anayostahili. Endapo hatatoa taarifa, BUWSSA italazimika kubadilisha gharama za matumizi stahiki ya mteja bila taarifa na mabadiliko hayo yataonekana kwenye Ankara ya maji ya mteja na mteja atalazimika kulipa deni husika ya maji.
  5. Wamiliki wa nyumba/majengo lazima watoe taarifa ndani ya kipindi cha siku 30 kama wapangaji wao wanatarajia kuhama.
  6. Mmiliki/wamiliki wa nyumba/jengo lililopangishwa wanatakiwa kuhakikisha Ankara za maji zinalipwa kila mwezi ili pindi mpangaji atakapoondoka bila kulipa deni la maji; wao wenyewe au  yeyote atakekutwa anatumia nyumba/jengo ambalo lina deni la maji lililotelekezwa na mpangaji au mtu aliyekuwemo awali atalazimika kulipa deni la nyuma ambalo halikulipwa na mpangaji au mtu aliyehama. BUWSSA ina haki ya kusitisha huduma ya maji mpaka deni linalodaiwa kwenye nyumba/jengo husika litakapolipwa kwa ukamilifu pamoja na gharama za urejeshaji huduma.
  7. Mteja ana haki ya kudai uchunguzi wa mita ya maji anapohisi kuna tatizo linalohusiana na utendaji kazi wa mita au usomaji usio sahihi.
  8. Mita itachunguzwa na kuthibitishwa mbele ya mteja kama iko sahihi au si sahihi. Na endapo mita itathibitika ina tatizo la kiufundi, BUWSSA italazimika kufanya matengenezo ya mita au kubadilisha mita hiyo na kumfungia mteja mita nyingine mpya.
  9. Mteja ana wajibu wa kulinganisha usomaji wa mita ulioko kwenye Ankara ya maji na ulioko kwenye mita yake kwa lengo la kujiridhisha kama matumizi ya maji aliyotozwa kwa mwezi husika ni halali au si halali au kama mita inasomwa au haisomwi. Na endapo mteja atagundua matumizi si halali au mita yake haisomwi analazimika kutoa taarifa haraka kwa Mkuu wa Kanda wa eneo anakoishi mteja au Kitengo cha Huduma kwa Wateja au Meneja Biashara katika Ofisi  ya BUWSSA.
  10. Marekebisho yote ya mita na majaribio yake yatafanywa bila malipo na BUWSSA isipokuwa kama uharibifu wa dira umesababishwa na mteja basi mteja atawajibika kulipia gharama hizo.
  11. BUWSSA ina wajibu wa kufanya makadirio ya gharama za matumizi ya maji kwa mazingira ambayo itajiridhisha kwamba maji yalitumika bila kuhesabiwa kwa usahihi kwenye mita wakati mita ikiwa mbovu au kwa mazingira ya kukwepa maji yasihesabiwe kupitia kwenye mita au kwa namna yoyote ambayo BUWSSA itajiridhisha kuwepo haja ya kukadiria gharama za matumizi ya maji kwa lengo la kufidia upotevu au wizi wa maji uliosababishwa na mteja.

NB: Kama italazimika kukadiria gharama za matumizi ya maji katika kipindi fulani, msingi wa ukadiriaji utakaotumika kutoza deni la maji utakuwa ni wastani wa matumizi sahihi ya maji kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu ya nyuma cha usomaji wa mita ya mteja.