TARATIBU ZA KUDAI NA KULIPA DENI LA MAJI

  1. Mteja lazima awe ameunganishwa kihalali katika miundombinu ya maji ya BUWSSA.
  2. Mamlaka ya maji Bunda inapinga vikali mteja kufanya malipo nje ya ofisi, wala kumpa mtumishi yoyote fedha kwa ajili ya malipo yoyote yanayohusu mamlaka.
  3. BUWSSA itatoa Ankara kila mwezi kwa wateja wote wanaotumia mita za maji pamoja na mawakala wote wa vioski/viula.
  4. Mteja hatamzuia afisa wa BUWSSA kuingia katika eneo lake kwa lengo la kusoma/kukagua dira na kufatilia ulipaji wa Ankara za kila mwezi.
  5. Mteja/Wakala yeyote ana wajibu wa kulipa deni la maji linalodaiwa kihalali na anatakiwa kulipa deni lote kila mwezi bila kulimbikiza.
  6. Kila mteja anawajibika kulipa deni lake lote la mwezi (current bill) ndani ya siku 15 kuanzia tarehe mosi ya mwezi unaofuata. Kama malipo yatakuwa hayajafanyika baada ya hizo siku 15, huduma ya maji inaweza kusitishwa wakati wowote. Aidha huduma ya maji inaweza pia kusitishwa kabla ya hizo siku 15 kufika endapo itabainika mteja anadaiwa deni la kipindi cha nyuma (arrears) lililolimbikizwa.
  7. BUWSSA inaweza kumtumia mteja ujumbe mfupi wa simu (SMSbilling) kumdai deni la maji au kama mteja hatapokea “SMS-billing” atalazimika kudai Ankara ya maji (water bill) kwa kufuatilia au kuwasiliana na ofisi za BUWSSA kwa kutumia Ankara yoyote ya zamani au kwa kutaja Akaunti namba yake ya maji (kama anaikumbuka) katika ofisi zetu za malipo.
  8. Mteja anaweza kulipa deni lake la maji kwa njia mbalimbali zifuatazo:
  9. Kwa mitandao ya simu za mkononi au Benki zilizoingia mkataba na Mamlaka pamoja na mawakala wa Benki hizo (NMB, CRDB). Malipo yote yalipwe kwa kutumia Control namba (kumbukumbu namba ya malipo).
  10. Mteja anatakiwa kurekebisha kumbukumbu zake za simu na kuitaarifu Mamlaka namba sahihi ya simu kwa ajili ya kupokea taarifa ya deni lake la maji kwa ujumbe wa simu (SMS-billing) kila mwezi.
  11. BUWSSA itadai deni la maji kwa mteja yeyote atakayehusika au atayekutwa kwenye nyumba, kiwanja/kitalu (plot) au eneo ambapo kuna mfumo wa maji bila kujali kwamba mteja aliyeko eneo hilo ni mmiliki wa eneo husika au ni mpangaji. Aidha, mwenye nyumba, kiwanja/kitalu, eneo au mpangaji wa eneo husika anapotaka kuhama au kutoka kwenye eneo hilo, atawajibika kulipa deni lote la maji kabla ya kuhama au kutoka eneo hilo. Ikiwa atahama au atatoka kwenye eneo hilo bila kulipa deni lote la maji linalodaiwa kwenye eneo husika, yeyote ambaye BUWSSA itamkuta kahamia eneo ambalo deni la maji halikulipwa atalazimika kulipa deni lote alilolikuta hapo ulipo mfumo wa maji.
  12. BUWSSA inaweza kupokea malipo ya madeni yaliyolimbikizwa kwa awamu kwa maombi ya mteja mwenyewe.
  13. Pale itakapo onekana inafaa BUWSSA inaweza kuingia mkataba na mkusanya madeni ili kudai madeni yake.
  14. Endapo mteja atakuwa na mashaka na deni au gharama za majisafi zilizotozwa kwenye Ankara yake atalazimika kufanya yafuatayo:
    • Kufika ofisi za BUWSSA na kuonana na watumishi wa Kitengo cha Mauzo na Huduma kwa Wateja ambao watachunguza uhalali wa deni husika na kumpatia mteja majibu sahihi.
    • Kumwandikia barua ya malalamiko Mkurugenzi Mtendaji kwa kuileta na kuikabidhi ofisi ya Masijala au kwa kuituma kupitia anuani ya Posta iliyoko kwenye Mkataba huu wa Huduma kwa Wateja, ambapo malalamiko yatafanyiwa uchunguzi na mteja atajibiwa kwa maandishi.