Mradi wa majisafi Nyamuswa, tumaini jipya kwa wakazi wa Nyamuswa na maeneo jirani

Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWSSA), siku ya tarehe 06/01/2025 ilitambulisha mradi wa maji kutoka Butiama hadi Nyamuswa, kwa wananchi wa Kata za Nyamuswa na Ketare, zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Bunda. BUWSSA ilitambulisha mradi huo kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Bunda Mh. Boniphace Getere, wakati alipokuwa akisikiliza na kutatua changamoto za wananchi wa Kata ya Nyamuswa.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa BUWSSA, Bi. Esther Gilyoma alisema Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya maji inatekeleza mradi wa kusambaza maji kupitia chanzo cha maji ya ziwa Viktoria. “Utekelezaji wa mradi huo, unatarajia kuanza tarehe 01/02/2025 na kukamilika tarehe 30/01/2026, kwa gharama ya zaidi ya TShs Bilioni 8.3 ambazo zinafadhiliwa na  Serikali kuu huku ukitekelezwa na Wakandarasi wawili ambao ni MOLI OIL MILLS pamoja na GAT ENGINEERING CO. LIMITED”. Alisema Bi. Gilyoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa BUWSSA amesema, vijiji vitakavyo nufaika na mradi huo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ni vijiji vitano (5), ambavyo ni kijiji cha Bukama, Makongo A, Makongoro B, Nyamuswa na Tiring’ati.

Naye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Ndugu Stafa Nashoni, aliwashukuru na kuwapongeza BUWSSA katika usimamizi wa mradi huo na aliahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha katika kuhakikisha wanatekeleza na kuukamilisha mradi huo kwa muda uliopangwa ili wananchi wa Nyamuswa na maeneo jirani waweze kunufaika na mradi huo.

Aidha Ndugu Nashoni alimpongeza na kumshukuru Mh. Mbunge kwa kuweza kusimamia na kuhakikisha mradi huo wa maji kutoka Ziwa Viktoria unaletwa katika Kata za Nyamuswa na maeneo Jirani.

Mradi wa majisafi kutoka Ziwa Victoria kupitia Wilaya ya Butiama hadi Nyamuswa unasimamiwa na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWSSA), chini ya Mkurugenzi Mtendaji wa BUWSSA Bi. Esther Gilyoma.

UPDATES : 23/01/2025

Mkataba wa utekelezaji wa Mradi wa Majisafi Nyamuswa umesainiwa rasmi tarehe 23/01/2025 katika ofisi za Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWSSA).

UPDATES : 28/01/2025

Mnamo tarehe 28/01/2025, Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew amelieleza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba mradi wa maji wa Nyamuswa unatarajiwa kuanza mwezi Februari 2025 na Mkandarasi ameshapatikana. Mhandisi Kundo alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Bunda Mhe. Boniphace Getere lililouliza ”Ni lini Serikali itatoa maji Ziwa Victoria kupitia mradi wa Mugango-Butiama-Kiabakari kuja Nyamuswa na kusambaa Jimbo zima la Bunda?’’

UPDATES: 26/04/2025

BI. ESTHER GILYOMA, ATOA SIKU 14 KWA MKANDARASI GAT ENGINEERING CO. LTD KUKAMILISHA UJENZI WA OFISI NDOGO NYAMUSWA

Mkurugenzi wa Mamlaka ya MajiSafi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWSSA) Bi. Esther Gilyoma, katika kuadhimisha sikukuu ya Muungano wa Tanzania amekagua maendeleo ya mradi wa maji wa Nyamuswa uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.

Bi.Gilyoma ametoa siku 14 ukamilishaji wa jengo la ofisi ndogo Nyamuswa uwe umekamilika kwa mkandarasi GAT ENGINEERING lengo likiwa kuruhusu kazi zingine za uchimbaji wa mitaro, ujenzi wa Matenki na ulazaji wa mabomba yenye urefu wa km 33 zianze mara moja.

Bi.Gilyoma amesema “Tunachohitaji ni kuona Wananchi wa Nyamuswa wanapata maji kufikia Mwezi wa kumi Mwaka huu, hatuna sababu ya kuchelewa na katika mradi unaotazamwa na serikali huu ni mmojawapo “

BUWSSA, kazi iendelee

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*