Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWSSA) Bi. Esther Gilyoma amesema Mamlaka hiyo imeidhinishiwa miradi yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 28 ndani ya miaka minne (4) ya uongozi wa Rais wa Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan hali iliyopelekea kufikia 85% ya upatikanaji wa huduma ya maji mjini humo kulinganisha na 60% mwaka 2021.

Bi. Esther Gilyoma – Mkurugenzi Mtendaji BUWSSA
Akizungumza na Waandishi wa Habari tarehe 06/03/2025 katika ukumbi wa Idara ya Habari – Maelezo Jijini Dodoma, Bi. Gilyoma ametaja miradi iliyoidhinishiwa fedha hizo kwamba ni Mradi wa ujenzi wa chujio la maji Nyabehu – Bunda, Mradi wa Miundombinu ya Majitaka Butakale, Ujenzi wa Mradi wa Maji Balili-Rubana-Kunzugu, Ujenzi wa Mradi wa Maji Manyamanyama-Mugaja, Ujenzi wa Mradi wa maji Misisi-Zanzibar, Mradi wa Kusambaza maji Wariku na Mradi wa kusambaza maji Kisangwa. Vilevile BUWSSA imeaminiwa kutekeleza mradi wa maji Nyamuswa unaogharimu zaidi ya TShs. Bilioni 8 ambapo utekelezaji wake umeshaanza.

Katika hatua nyingine, Bi. Gilyoma amewasisitiza wananchi wa Mji wa Bunda na Watanzania kwa ujumla wanaohitaji huduma ya maunganisho mapya ya maji kufuata utaratibu wa kupata huduma hiyo kwani vishoka wengi hutumia mwanya huo kuwatapeli wananchi kwa kigezo cha kuwaletea maji kwa haraka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya BUWSSA Mhe. Joshua Chacha Mirumbe amemshukuru Mhe. Rais kwa fedha nyingi alizozielekeza katika miradi ya majisafi na majitaka mjini Bunda na hivyo kumaliza kwa kiasi kikubwa changamoto ya ukosefu wa maji na uzalishaji wa maji machafu kwa wakazi wa maeneo hayo.

Mhe. Joshua Chacha Mirumbe – Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi BUWSSA
Mhe. Mirumbe ameipongeza Wizara ya maji kupitia Mhe. Jumaa Aweso na watendaji wote kwa kazi kubwa iliyofanyika katika Mji wa Bunda ndani ya miaka minne huku akieleza kuridhishwa na utendaji kazi wa Mkurugenzi Mtendaji wa BUWSSA kwani ndani ya Miaka mitatu ya uongozi wake katika Mamlaka hiyo, BUWSSA imepanda Daraja kutoka Daraja ‘C’ Kwenda Daraja ‘B’ na kuifanya Mamlaka iwe na uwezo wa kujiendesha yenyewe.
#BUWSSA, Kazi Iendelee
Leave a Reply